LIMSpec Wiki

Utungo uliotokana na kutungwa kwa Shanga

Tungo ni neno au nomino inayotokana na kitenzi "tunga". Kutunga ni kuweka/kushikamanisha vitu pamoja kwa kutumia kitu kama kamba au uzi kwa kupitishia ndani yake. Kwa mfano, unaweza kutunga vitu kama samaki, shanga, simbi na kadhalika.

Unaposhikamanisha vitu pamoja tunapata kitu kinachoitwa utungo (mmoja) au tungo (nyingi).

Uchambuzi

Katika taaluma ya lugha (sarufi) tuna dhana hiyohiyo ya kuweka/kushikamanisha vitu pamoja, yaani kupanga/kuweka pamoja vipashio vya lugha ili kujenga kipashio kikubwa zaidi.

Tungo ni nini?

Neno tungo katika lugha ya Kiswahili, hasa kwa upande wa sarufi, lina maana ya neno au mpangilio wa maneno unaotoa taarifa fulani. Taarifa hiyo inaweza kuwa kamili au la. Mfano: Yeye anayesoma.... Yule anajua kuandika. Lakini lazima kuwe na mpangilio kamili katika muundo mzima wa kisarufi.

Aina za tungo

  1. Kigezo cha viwango
  2. Kigezo cha muundo
  3. Kigezo cha maana

Tungo kishazi

Kishazi ni tungo yenye kitenzi ambacho chaweza kujitosheleza na kukamilisha ujumbe uliokusudiwa na mzungumzaji au kuwa na kitenzi kisichoweza kujitegemea.

Sifa za tungo kishazi

  • Kishazi hupatikana katika/ndani ya sentensi.
  • Lazima kishazi kiwe na kitenzi: sehemu yoyote ya sentensi isiyo na kitenzi, haiwezi kuwa kishazi. Kishazi huru hutawaliwa na kishazi kikuu, na kishazi tegemezi hutawaliwa na kishazi tegemezi.
  • Baadhi ya vishazi huweza kujitegemea kama sentensi hata vikiondoshwa katika muktadha wa sentensi kuu. Kishazi kinachoweza kujisimamia kama sentensi huitwa kishazi huru kikiwa ndani ya sentensi kuu na huitwa “sentensi sahili” kikiwa sentensi inayojitegemea.
  • Baadhi ya vishazi haviwezi kujitegemea kama sentensi ikiwa vitaondoshwa katika muktadha wa sentensi kuu.
  • Vishazi vingi, hata vishazi huru huwa na kiima dhahiri.
  • Kishazi kwa kawaida, hasa kishazi huru, huwa na kitenzi kimoja kikuu.
  • Kitenzi hicho huweza kuandamana na kitenzi kisaidizi. Pia, kitenzi katika kishazi huweza kuwa kitenzi kishirikishi.
  • Kishazi hutekeleza majukumu mbalimbali ya kisarufi.
  • Tofauti kati ya kishazi na sentensi ni kwamba kishazi hupatikana ndani ya sentensi lakini sentensi hujisimamia kimuundo na kimaana. Kishazi huwa na kiarifu kimoja na kiima kimoja, Lakini sentensi huweza kuwa na kiima kimoja.

Aina za tungo kishazi

Kuna aina mbili za tungo kishazi nazo ni:

  • 1. kishazi huru
  • 2. kishazi tegemezi

Kishazi huru

Kishazi huru ni kishazi kinachotawaliwa ka kitenzi kikuu, ambacho kwa kawaida hutoa ujumbe kamili usiohitaji maelezo zaidi ya kukamilisha maana.

Kishazi tegemezi

Kishazi tegemezi ni kishazi kinachotawaliwa kwa kitenzi kisaidizi, ambacho muundo wake hukifanya kutegemea kitenzi cha kishazi huru ili kuweza kutoa ujumbe uliokusudiwa.

Sifa za kishazi tegemezi
  • Kishazi tegegemezi hutoa maana kamili kinapoandamana na kishazi huru.
  • Kishazi tegemezi kinaweza kufutwa katika sentensi bila kuharibu maana ya sentensi nzima.
  • Kishazi tegemezi hutambulishwa na viambishi vya utegemezi
Aina za vishazi tegemezi

Kuna aina mbili za vishazi tegemezi nazo ni:

  • 1. Vishazi tegemezi vivumishi.
  • 2. Vishazi tegemezi vielezi.

Tazama pia

Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Tungo kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.