Practical Applications of a SDMS (Scientific Data Management System)

Hariri viungo
Papa Fransisko akiendesha Misa ya kuanzia rasmi huduma yake kama askofu wa Roma na mkuu wa Kanisa Katoliki duniani kote, tarehe 19 Machi 2013.
Hii ni sehemu ya mfululizo kuhusu
Kanisa Katoliki
Imani

Umoja wa Mungu
Utatu (Baba, Mwana, Roho Mtakatifu)
Umwilisho Maisha ya Yesu
Msalaba Ufufuko Kupaa
Historia ya Wokovu Ufunuo
Biblia Mapokeo Ualimu Dogma
Neema Dhambi Wokovu Sakramenti
Watakatifu Bikira Maria

Muundo

Papa: Fransisko
Urika wa maaskofu Mitaguso mikuu
Kundi la Makardinali
Kanisa la Kilatini
Makanisa Katoliki ya Mashariki

Historia

Historia Ukristo
Ukatoliki Mlolongo wa Kitume
Sifa nne za Kanisa Utetezi Ekumeni
Maisha ya kiroho Amri Kumi Utawa
Sala Falsafa Teolojia
Muziki Sanaa Sayansi

Ibada

Liturujia Mwaka wa Kanisa
Ekaristi Liturujia ya Vipindi

Mapokeo ya liturujia

Liturujia ya Kilatini (Roma Liturujia ya Trento Milano Toledo Braga Lyon Canterbury)
Liturujia ya Armenia Liturujia ya Misri
Liturujia ya Ugiriki Liturujia ya Antiokia
Liturujia ya Mesopotamia


Kanisa Katoliki ni jina linalotumika kwa maana mbalimbali, lakini hasa kumaanisha Kanisa la Kikristo linalokubali mamlaka ya kiroho ya Papa wa Roma kama mkuu wa urika wa maaskofu juu yake lote.

Ndilo kubwa kabisa kati ya madhehebu yote ya dini hiyo, likikusanya nusu ya wafuasi wote wa Yesu.

Hata hivyo, Wakristo wa madhehebu mengine wanaokubali kanuni ya imani ya Nisea-Konstantinopoli wanatafsiri tofauti sehemu yake inayokiri Kanisa la kweli kutambulishwa na sifa nne, ya tatu ikiwa kwamba ni katoliki: "Tunasadiki Kanisa moja, takatifu, katoliki, la Mitume".

Kanisa Katoliki, likiwa na miaka karibu elfu mbili, ni kati ya miundo ya zamani zaidi iliyopo duniani na imechangia kwa kiasi kikubwa ustaarabu wa Magharibi, ingawa tangu mwishoni mwa Karne za Kati athari yake inazidi kupungua, ilivyo wazi leo hasa katika masuala yanayohusu jinsia na uzazi.

Imani ya Kanisa hilo inatokana na ufunuo wa Mungu ulivyotolewa kwa Israeli na ulivyokamilishwa na Yesu ambaye alimtambulisha kama Baba na alilianzisha kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetumwa naye juu ya Mitume wake siku ya Pentekoste mwaka 30 (au 33) BK.

Ni imani inayoungamwa katika ubatizo, sakramenti ya kwanza na mlango wa sakramenti nyingine sita: kwamba Mungu ni mmoja tu katika nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Imani hiyo inatakiwa kutekelezwa katika maadili maalumu yanayotegemea hasa upendo ambao ndio adili kuu na uhai wa mengine yote.

Kutokana na juhudi za kutekeleza matendo ya huruma kwa yeyote mwenye shida, Kanisa Katoliki linatoa huduma za elimu na afya kuliko taasisi nyingine yoyote duniani kote.

Kama vielelezo vya utakatifu ambao waamini wote wanaitiwa, Kanisa linapendekeza watu wa Agano la Kale na wa Agano Jipya, hasa Bikira Maria, lakini pia wale waliojitokeza zaidi katika historia yake kama watakatifu.

Baadhi yao wana wafuasi wengi wanaounda familia za kiroho, mara nyingi kama mashirika ya kitawa yenye karama mbalimbali.

Maana ya jina

Kanisa

Neno Kanisa maana yake ni “Mkusanyiko”: ndani yake Roho Mtakatifu anaunganisha na Yesu na kati yao wale waliopokea Neno la Mungu na sakramenti zake. “Bwana alilizidisha Kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa… Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja” (Mdo 2:47; 4:32). Ndio tokeo la ombi la Yesu: “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako, hao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma” (Yoh 17:21). Kumbe utitiri wa madhehebu yaliyotenganika unaleta picha ya “mtawanyiko” ambayo inakwaza ulimwengu usisadiki. “Kila mtu wa kwenu husema, ‘Mimi ni wa Paulo’, na, ‘Mimi ni wa Apolo’, na, ‘Mimi ni wa Kefa’, na, ‘Mimi ni wa Kristo’. Je, Kristo amegawanyika?” (1Kor 1:12-13).

Kwa imani hiyo, Kanisa si kundi la binadamu tu, tunaloweza kulianzisha kama vile chama, timu n.k. Kanisa ni fumbo la Mwili wa Kristo unaohuishwa na Roho Mtakatifu. Kama Yesu linaonekana upande wa ubinadamu tu, kumbe linaunganisha utu na Umungu. Baba “alivitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya Kanisa, ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote” (Ef 1:22-23).

Hivyo hatuwezi kuambatana na Yesu kwa kulikataa Kanisa, kwa kuwa hao wawili ni mwili mmoja, kama Bwanaarusi na Bibiarusi. “Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, ‘Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja’? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe” (Math 19:4-6). “Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa” (Ef 5:32).

Kwa sababu hiyo Kanisa ni muhimu kwa wote kwa kuwa ndilo ishara na chombo cha umoja wa watu na Mungu na kati yao. Yesu “aliwapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba. Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwao wale waliokuwa karibu. Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja” (Ef 2:16-18).

Katoliki

Halafu neno "katoliki" linatokana na kivumishi cha Kigiriki καθολικός (katholikòs), lenye maana ya «kamili, kadiri ya utimilifu», kinyume cha «vipandevipande».

Tunalikuta kwa mara ya kwanza katika maandishi ya Ignas wa Antiokia kwa Wakristo wa Smirna mwanzoni mwa karne II: «Alipo Yesu Kristo ndipo lilipo Kanisa Katoliki» (Ad Smyrnaeos, 8).

Ndivyo alivyolitofautisha na makundi madogomadogo yaliyokuwa yameanza kujitenga nalo.

Imani yake kuhusu fumbo lake kama ushirika

Kanisa hilo linaamini kuwa ndani yake linadumu moja kwa moja Kanisa pekee lililoanzishwa na Yesu Kristo ambalo wanaunganishwa nalo wale wote wanaobatizwa katika madhehebu yoyote.

Tofauti kati yao ni kwamba baadhi (Wakatoliki) wana ushirika kamili nalo, wakati wengine (hasa Waorthodoksi, Waorthodoksi wa Mashariki na Waprotestanti) wana ushirika nalo kwa viwango mbalimbali, kadiri wanavyokubali mafundisho, sakramenti na uongozi wake.

Hatimaye, Kanisa hilo linaamini kuwa wale wote wasiobatizwa wanaitwa na Mungu kufanya hivyo na kujiunga nalo ili wafikie wokovu ulioletwa na Yesu Kristo.

Sababu ni kwamba wokovu unapatikana kwa Yesu tu, anayeishi katika Kanisa lake. Hata hivyo Roho Mtakatifu anaweza akaongoza mtu asiyewajua bila kosa lake aungane nao kiroho kwa kumlenga Mungu na kujitahidi kumtii kwa moyo wote. “Tunamtumaini Mungu aliye hai, aliye Mwokozi wa watu wote, hasa wa waaminio” (1Tim 4:10). “Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye… Twaamini kwamba tutaokoka kwa neema ya Bwana Yesu vilevile kama wao” (Mdo 10:34-35; 15:11).

Lakini mtu akijua Kanisa ni la lazima kwa wokovu asiingie au ajitenge nalo hawezi kuingia mbinguni. “Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe” (1Tim 4:1-2). “Watoto, ni wakati wa mwisho. Na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho. Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu” (1Yoh 2:18-19).

Si kwamba anayejiunga na Kanisa na kudumu ndani yake ana hakika ya kuingia mbinguni, kwa sababu kama haongozwi na Roho Mtakatifu kuishi kadiri ya ubatizo wake atahukumiwa na Mungu vikali zaidi kwa kuchezea neema kubwa hivi. “Kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi” (Lk 12:48).

Ushirika wa watakatifu maana yake Wakristo, kwa kushiriki mafumbo matakatifu wanaunda ndani ya Kristo mwili mmoja, ambamo waadilifu waliopo duniani, marehemu wa toharani na wenye heri wa mbinguni wanaunganishwa na upendo wafaidike na mema ya kila mmoja. “Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia” (Rom 14:8-9). “Kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho. Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake” (1Kor 12:26-27). Dhambi yoyote kubwa inatutenga na ushirika huo kama Yesu alivyosema, “Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa” (Yoh 15:1-2). Lakini “Mungu aweza kuwapandikiza tena... Kwa sababu karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake” (Rom 11:23,29).

Aina za waumini

Kanisa limepewa na Yesu wahudumu wenye daraja takatifu wanaoitwa wakleri; waamini wengine wanaitwa walei. Kutoka pande hizo mbili wanapatikana watawa waliowekwa wakfu kwa namna ya pekee kwa kushika mashauri ya Kiinjili. Yesu “alipanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri” (Mk 3:13-14). “Walipoingia, wakapanda orofani, walipokuwa wakikaa; Petro, na Yohane, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo. Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake” (Mdo 1:13-14).

Yesu amejenga Kanisa lake imara juu ya Mtume Petro, alichunge lote kwa niaba yake. Papa kama Askofu wa Roma ndiye mwandamizi wa Petro na mkuu wa kundi zima la Maaskofu, waandamizi wa Mitume. “Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda” (Math 16:18). “Atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba. Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba” (Math 7:24-25). Historia ya miaka elfu mbili sasa imedhihirisha ukweli wa maneno hayo.

Papa amejaliwa na Mungu mamlaka kamili juu ya waamini wote awafungulie ufalme wa mbinguni, kama Yesu alivyomuambia Petro: “Nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni, na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni” (Math 16:19). “Nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako” (Lk 22:32). “Lisha wanakondoo wangu… Chunga kondoo zangu… Lisha kondoo zangu” (Yoh 21:15-17).

Maaskofu wote wamerithi mamlaka ya Mitume kwa kufundisha, kutakasa na kuongoza Kanisa lote pamoja na Papa na chini yake. Wale waliokabidhiwa jimbo fulani ni msingi wa umoja kwa waamini wao na kati yao na Kanisa lote duniani. “Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe” (Mdo 20:28).

Maaskofu wanasaidiwa kwanza na mapadri katika uchungaji, halafu na mashemasi katika utumishi. “Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye: lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia” (1Pet 5:1-2). “Paulo na Timotheo, watumwa wa Kristo Yesu, kwa watakatifu wote katika Kristo Yesu, walioko Filipi, pamoja na Maaskofu na mashemasi” (Fil 1:1).

Bila Maaskofu, mapadri na mashemasi, Kanisa lisingekuwepo kwa sababu uhai wake unategemea kabisa ekaristi iliyokabidhiwa kwao. “Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja” (1Kor 10:16-17). Bila ekaristi tusingekuwa Kanisa, bali jumuia tu, kama madhehebu mengi yaliyojichagulia viongozi wasioshirikishwa hizo daraja takatifu kwa kuwekewa mikono na mwandamizi wa Mitume. “Uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu” (2Tim 1:6). “Nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru” (Tit 1:5). “Usimwekee mtu mikono kwa haraka” (1Tim 5:22).

Walei wanaitwa na Mungu kuratibu malimwengu yote yafuate matakwa yake. “Wapeni wote haki zao; mtu wa kodi, kodi; mtu wa ushuru, ushuru; astahiliye hofu, hofu; astahiliye heshima, heshima” (Rom 13:7). “Uwakumbushe watu kunyenyekea kwa wenye uwezo na mamlaka, na kutii, na kuwa tayari kwa kila kazi njema” (Tit 3:1). “Kwa sababu ndiyo mapenzi ya Mungu, kwamba kwa kutenda mema mzibe vinywa vya ujinga vya watu wapumbavu; kama walio huru, ila wasioutumia uhuru huo kwa kusitiri ubaya, bali kama watumwa wa Mungu” (1Pet 2:15-16).

Watawa wanashika hasa mashauri ya useja mtakatifu, ufukara na utiifu ambayo msingi wake ni maisha na mafundisho ya Yesu kadiri ya Injili. “Wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee” (Math 19:12). “Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate” (Math 19:21). “Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo” (Yoh 15:14).

Uenezi wake

Asilimia ya Wakatoliki waliobatizwa kati ya wakazi wa kila nchi.

Kati ya madhehebu ya Kikristo, Kanisa Katoliki linaundwa na waamini 1,390,000,000 (31 Desemba 2022), yaani nusu ya wafuasi wote wa Yesu, na 17.67 % ya binadamu wote[1], likiwa na asilimia kubwa ya waamini kati ya wananchi wa Amerika (64.1%) na Ulaya (39.6%).

Hata hivyo Wakatoliki kwa muda mrefu sasa wanaongezeka hasa katika mabara ya Afrika (273,000,000, 19.4% za wakazi wote) na Asia (153,355,000, 3.3% za wakazi wote)[2].

Miundo yake

Kanisa Katoliki linaishi katika majimbo 3,040, ambayo kwa kawaida yanaongozwa na Maaskofu (kwa jumla wako 5,353) wakisaidiwa na mapadri (407,730) na mashemasi, ambao baadhi yao wanajiandaa kupata upadrisho na 50,150 ni wa kudumu[3].

Kati ya majimbo hayo, mengi yanafuata taratibu za Kanisa la Kilatini, ila kuna mengine yanayofuata taratibu za Makanisa Katoliki ya Mashariki. Ni kwamba, tukitaka kutumia maneno kikamilifu tunapaswa kujua kwamba Kanisa la Kiroma si lile lote lililo chini ya Papa, bali lile tu linalofuata mapokeo ya Roma kuanzia ibada zake zinazotegemea lugha ya Kilatini. Kumbe yapo mengine (kama Kanisa Katoliki la Kiethiopia) ambayo hukubali pia uongozi wa Papa ila hufuata mapokeo ya Kiorthodoksi.

Asili ya makanisa hayo ni katika majaribio ya kuunganisha tena Makanisa ya Kiorthodoksi na lile la Roma; kwa kawaida majaribio hayo hayakufaulu, ila yalivuta maaskofu na Wakristo wachache. Maaskofu hao pengine walipewa na Papa cheo cha Patriarki (wa Aleksandria, wa Antiokia n.k.) kwa kushindana na Mapatriarki wa Makanisa ya kale. Lakini zipo nchi kadhaa ambako Wakristo wengi wa mapokeo ya Kiorthodoksi hufuata uongozi wa Papa kama kule Lebanon, Iraq na wengi kidogo katika nchi ya Ukraina.

Katika nchi kadhaa Makanisa mbalimbali ya Kikatoliki yanaishi kandokando, kwa mfano Misri kuna Kanisa Katoliki la Wakopti, Kanisa Katoliki la Kimelkiti, Kanisa Katoliki la Armenia, Kanisa Katoliki la Wakaldayo na la Kilatini. Mapadri (lakini si maaskofu) Wakatoliki wa mapokeo ya Kikopti, ya Kigiriki, ya Kiarmenia na ya Kikaldayo wanaweza kuwa na ndoa na huendesha Misa katika taratibu zao za kale; kumbe mapadri Walatini hawawezi kuwa na ndoa na hufuata liturujia ya Roma.

Wote hao hukubali uongozi wa Papa bila kushindana, yaani wengine wanahudumia Wakatoliki wa mapokeo ya Kikopti, wengine wale wa mapokeo ya Kigiriki, wengine wale wa mapokeo ya Kiarmenia, wengine wale wa mapokeo ya Kikaldayo na wengine wale wa mapokeo ya Kiroma, hasa wahamiaji kutoka nchi nyingine.

Majimbo yote yanagawanyika katika parokia zinazoongozwa na padri anayeitwa paroko.

Kati ya waamini, ambao wengi kabisa kati yao ni wale wa kawaida wanaoitwa walei, wana nafasi ya pekee wamonaki na watawa wengine ambao wanaishi kwa mitindo mbalimbali iliyostawi katika historia ya Kanisa ili kumfuata Yesu kwa karibu zaidi katika useja mtakatifu, ufukara na utiifu, kadiri ya karama maalumu. Masista ni 608,958 hivi na mabruda 49,774[4].

Tanbihi

Marejeo

  • "Catechism of the Catholic Church". Libreria Editrice Vaticana. 1994. Iliwekwa mnamo 1 Mei 2011.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  • Bunson, Matthew (2008). Our Sunday Visitor's Catholic Almanac. Our Sunday Visitor Publishing. ISBN 1-59276-441-X.
  • Gale Group. (2002) New Catholic Encyclopedia, 15 vol, with annual supplements; highly detailed coverage
  • Papa Yohane Paulo II, (2006) He Gave Them the Law of Life as Their Inheritance, in:Man and Woman He created Them. A Theology of the Body, transl. M. Waldstein, Boston: Pauline Books and Media, pp. 617–663 ISBN 0-8198-7421-3
  • Smith, Janet, ed. (1993) Why "Humanae Vitae" Was Right, San Francisco: Ignatius Press.
  • Smith, Janet (1991) "Humanae Vitae", a Generation Later, Washington D.C.: Catholic University of America Press,
  • Stewart, Cynthia. (2008) The Catholic Church: A Brief Popular History 337 pages
  • Vatican, Central Statistics Office (2011). Annuario Pontificio (Pontifical Yearbook). Libreria Editrice Vaticana. ISBN 978-88-209-7908-9.

Viungo vya nje

WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Makala hii kuhusu Kanisa Katoliki bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kanisa Katoliki kama historia yake au maelezo zaidi?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa .